MBUNGE WA JIMBO LA CHILONWA WILAYANI CHAMWINO AWAHAKIKISHIA WAKAZI WA KATA YA IKOWA UPATIKANAJI WA MAJI SAFI NA SALAMA.
Na Stephen Jackson
Halmashari ya wilaya ya chamwino mkoani Dodoma Inaendelea na jitihada za kutatua kero za wananchi wake katika upatikanaji wa huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo maji safi na salama.
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa jimbo la Chilonwa Mheshimiwa Joel Mwaka Makanyaga, alipotembelea kata ya Ikowa tarehe 20/12/2017 kwa lengo la kujionea hali ya upatikanaji wa huduma ya maji pamoja na ufanisi wa paneli za umeme jua zilizofungwa katika zahanati ya Ikowa, ikiwa ni sehemu ya majukumu yake ya kawaida. Aidha Ndugu Joel Makanyaga kupitia ukurasa wake wa facebook amebainisha kuwa mikataba ya uchimbaji kisima cha Ikowa na uwekaji pampu katika kisima cha Udinde ipo mbioni kukamilika ambapo shughuli za miradi hiyo zinatarajiwa kuanza muda wowote. ”Siku chache zijazo kisima kitachimbwa Ikowa na pia kisima cha Udinde kitawekewa pump” Anaandika Mhe. Joel Mwaka Makanyaga.
Aidha Mheshimiwa Makanyaga ameongeza kuwa, miradi hiyo itahusisha pia ujenzi wa malambo ya maji na majosho kwaajili ya kuhudumia mifugo. Hivyo basi, kukamilika kwa miradi hiyo kutaweza kutatua kero ya huduma za maji kwaajili ya matumizi ya kawaida ya kibinadamu pamoja na mifugo.
Comments