Na Stephen Jackson
Matukio ya kuvunjika kwa ndoa siku hizi ni wimbo wa kawaida sana masikioni mwetu takribani kila pembe ya dunia. Mara nyingi zinashudiwa ndoa kadhaa zikivunjika huku nyingine zikirejea kwenye mstari. Je,ulishawahi kujiuliza nini sababu hasa inayopelekea hali hiyo? Ungana nami leo katika makala hii ambayo naamini ni darasa huru litakalokujuza mambo mengi kuhusu sababu za kuvunjika na kurejea kwa ndoa hizo.
Kwa kawaida ndoa ni muunganiko wa hiari kati ya mwanamke na mwanaume waliokubaliana kuishi pamoja katika maisha yao yote.Kutokana na tafsiri hiyo taratibu za kufunga ndoa huzingatiwa,ikiwa ni pamoja na kuwekwa ushahidi mkubwa kabla,wakati na baada ya kufungwa kwa ndoa. Sababu kubwa ya kuweka ushahidi mkubwa ni kutokana na unyeti wa jambo lenyewe ambalo kwa kawaida hufanyika mara moja tu katika uhai wa mwanadamu.Hata hivyo kutokana na tofauti za kiutamaduni ndoa yaweza kufungwa zaidi ya mara moja kwa mtu huyo huyo, mathalani mtu anapofiwa na mwenzi wake wakati umri wake unaruhusu kuendelea na maisha ya ndoa, mtu anaweza kufunga ndoa tena. Swala la msingi ni kwamba kila ndoa inayofungwa hukusudiwa kudumu kwa maisha yote ya wanandoa hao ambapo kudumu kwenyewe kunatengemea mambo yafuatayo; Kwanza wanandoa waungane kwa hiari, na wasiwe na vigezo vingine tofauti na upendo, pili angalau wawe na desturi zinazolingana, tatu imani zao zifanane, nne hisia zao ziendane, tano shughuli zao zishabihiane, sita ndugu zao wapendane saba jamaa na marafiki wasiwachonganishe n.k.
Hata hivyo hutokea mara chache sana vigezo hivyo kuwiana na ndiyo sababu watu wengi huangalia walau vigezo vichache tu. Madhara ya kufanya hivyo ni kujiamini kuwa mwanandoa atavumilia madhaifu yatakayojitokeza kutokana na baadhi ya vigezo kutowiana kabisa. Katika msingi huu uvumilivu unasimama kama daraja la kuwasaidia wanandoa kupita hasa wanapokumbana na misukosuko ya maisha kama vile kuyumba kwa kipato cha familia, magonjwa, na matatizo mengine ya kifamilia. Hiki ndicho kipindi ambacho ,ndoa huingia dosari ambazo kimsingi hakuna njia yoyote ya kuziondoa isipokuwa kuzivumilia dosari hizo na kuzichukulia kama sehemu ya maisha huku mwenye dosari hizo akijitahidi kujirekebisha.
Wapo wanandoa ambao wanaweza kuvumilia na wasiovumilia kabisa,hivyo ndoa hugeuka kuwa tatizo na kuzua balaa katika familia hasa pale mwanandoa mmojawapo anaposhindwa kuvumilia na kuanza kutafuta suluhisho nje ya ndoa.Kimsingi hakuna suluhisho nje ya ndoa baada ya ndoa kufungwa,isipokuwa ni watu wawili tu (wanandoa) ndio wenye mamlaka na uwezo wa kutatua tofauti zao.Wengi wamekuwa wakiwakimbilia viongozi wa dini zao wakiwabebesha mizigo ya migogoro yao ya ndoa wakidhani wanaweza kusaidiwa,badala yake wamekuwa wakiongeza chuki katika familia zao hasa viongozi wao wanapogundua makosa ya mmoja wao na kumweleza ukweli.Hata hivyo kwa kiasi fulani baadhi ya viongozi wamekuwa wakifanikisha kusuluhisha migogoro ya ndoa hasa inayohusika na tamaa ya mali na migongano ya maslahi kuliko ile inayohusu masuala ya wanandoa wenyewe mathalani kugundulika kwa nyumba ndogo n.k. Kutokana na hali hiyo kila mwanandoa anapaswa kutunza moyoni madhaifu yote anayoyagundua kwa mwenzi wake,na kumshauri kwa hekima namna ya kufanya ili kuepukana na hali hiyo.
Mara nyingi wanaume huwa ni watu wasiopenda kudharauliwa na wanawake kwa namna yoyote ile,hivyo mwanamke anapoonesha dharau moja kwa moja hupunguza au kuondoa kabisa upendo wa mke na mume yaani upendo wa Ndoa na matokeo yake mwanaume huanza kuabudu Ndoa badala ya kuifurahia.Baadhi ya wanaume huanza kutafuta faraja kwa wanawake wa nje ya Ndoa ambao mara nyingi hujifanya ndio walimu wa mapenzi kwa kuzingatia mambo yote ambayo mwanaume anatakiwa kufanyiwa.Huu ndio huwa mwanzo wa kuvunjika kwa Ndoa nyingi.
Wanandoa walioachana wanaweza kurudiana kirahisi ikiwa jamii yao haijui sababu za kuachana kwao,kwani ni maamuzi yao wawili kuliko Ndoa zinazovunjika Kutokana na kasoro za wanandoa kuanikwa hadharani. Hii ni kwa sababu wanandoa huona haya dhidi ya kauli mbaya za kujiapiza kuwa hawezi kuishi tena na mwenzi wake.
Hivyo basi ikiwa mtu amefunga ndoa yampasa kutambua kuwa yeye ndiye mwenye dhamana ya kulinda kiapo chake na si mwingine yeyote.Pia pamoja na kiapo hicho anapaswa kufahamu kuwa kutangaza udhaifu wa mwenzi wake ni ishara ya kujitambua kuwa yeye ni adui wa kwanza wa ndoa yake.
Ikiwa unapenda ndoa yako isivunjike ni lazima utambue kuwa ndoa hiyo itakuwepo hadi mwisho wa uhai wako hivyo kutengana ni kujipotezea muda wa kufanya mambo ya msingi na mpenzi wako, pili unapaswa kuamini kuwa hakuna suluhisho nje ya ndoa, tatu samehe makosa yote ya mpenzi wako hata kama ni makubwa kiasi gani.
Ikiwa tayari umetengana na mpendwa wako ni lazima ujitahidi kufanya yafuatayo; kama uliachwa unapaswa kurudi na kuomba msamaha,pili ni lazima uthibitishe kuwa makosa ya awali hayatojirudia, tatu ukifanikiwa ni lazima urudi mapema zaidi na ujitahidi kumfurshisha mwenzi wako kwa kila kitu.
Ikiwa ulimuacha mke au mume wako na unataka kumrudia ni lazima kwanza umsamehe yote aliyokukosea pili fanya mawasiliano naye na kumueleza dhamira yako, tatu,thibitisha kuwa hautomuhukumu kwa makosa yaliyopita,akikubali ujitahidi kuanza naye maisha mapya.
Mpendwa msomaji ni matumaini yangu kuwa umeelewa somo la leo.
Ikiwa una maoni yoyote tafadhali tutumie ujumbe kwa simu namba 0755 800 798.
Comments